Seminari Kuu ya Kitaifa ya Familia Takatifu Mwendakulima yaadhimisha Misa Takatifu kumuombea MAREHEMU BENEDICTO XVI PAPA
Masomo:Somo I: Hek. 3: 1 – 9Somo II: Rom. 8: 31 – 35; 37 – 39Injili: Lk. 12: 35 – 40
Leo Waseminaristi na Walezi wa Seminari ya Familia Takatifu – Mwendakulima wameunganika na Kanisa zima kumwombea Benedicto XVI Papa, aliyefariki dunia Desemba 31, 2022 huko Vatican City; Na anazikwa leo, 5 Januari, 2023. Mungu ampe raha ya milele.
Katika homilia yake Pd. Dkt. Philipo Kireti alilielezea fumbo la Kifo kama mwanzo wa Maisha mapya; ndiyo kusema sisi waamini wakatoliki tunaamini, kifo ni mwanzo mpya wa maisha ya milele. Hivyo Benedicto XVI Papa anaanza maisha mapya (ulimwengu wa roho) katika Kristo. Kama tunavyoambiwa katika kitabu cha Hekima: “Roho zao wenye haki zimo mikononi mwa Bwana, baada ya kujaribiwa na kuonekana kuwa wanastahili” (Hek. 3).
Benedicto XVI Papa ambaye jina lake la kubatizwa ni Joseph Alois Ratzinger, alizaliwa mwaka 1927 na kufariki Desemba 31, 2022. Amekuwa Baba Mtakatifu tangu 2005 hadi 2013 alipostaafu.
Tunamshukuru Mungu kwa nguvu na mwanga wa Roho Mtakatifu aliomjalia katika kipindi alichoongoza Kanisa Katoliki kama Papa. Kilikuwa ni kipindi kigumu na chenye changamoto nyingi zilizotishia kuligawanya kanisa. Kulikuwa na malumbano mengi kuhusu nidhamu na uadilifu katika uongozi wa juu wa Kanisa. Na pia, maadui wa kada mbalimbali, waliojaribu kusababisha ashindwe katika kufanya utume wake kama kiongozi mkuu wa Kanisa.
Pamoja na changamoto hizi, Benedicto XVI Papa alidumu katika imani na mapendo kwa Kanisa. Alimtegemea Kristo na kumfanya kuwa kinga yake, kama anavyosema Mt. Paulo katika Waraka wake kwa Warumi: “Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga?” “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu mwenyewe huwaondolea hatia” (Rom. 8:33).
Aidha, Pd. Dkt. Philipo Kireti ameelezea Maisha na umahiri wa Benedicto XVI katika kufundisha, kuilinda na kuitetea imani ya Kristo Yesu akisema: Benedicto XVI Papa alitoa maisha yake kwa moyo mkuu kulihudumia Kanisa. Tangu alipopewa Upadre June 1951, alifundisha elimu kumhusu Mungu (Theology) katika vyuo vikuu vya Freising, Bonn, Münster na Tübingen; kuwafanya watu wajue ukweli kumhusu Mungu.
Anaendelea kusema kwamba, baada ya kufanywa Askofu Mkuu wa Munich na Freising mwaka 1977, mwaka 1981 Novemba 25 aliteuliwa na Yohane Paulo II Papa kuwa msimamizi wa Congregatio inayosimamia mafundisho ya Kanisa kuanzia mwaka 1978 – 2005.
Vilevile, Pd. Dkt. Kireti alikazia kuwa Benedicto XVI Papa (wakati huo Ratzinger Cardinali), alizuia mafundisho yote ya Theolojia yaliyokuwa na utata yasifundishwe kwenye Seminari Kuu wala vyuo vikuu vya Kanisa. Na alikemea na kukosoa mitazamo ya kitheolojia iliyokuwa inamlengo tofauti na Kanisa kama vile Liberation Theology na tulishuhudia vitabu vingi vikiondolewa katika maktaba (huu ni ushuhuda alioushuhudia Pd. Dkt. Kireti wakati akisoma Roma).
Pia kwa upande mwingine, waliokuwa wanampinga walitambua na kukubali uwezo wake wa akili na uelewa wa kujadili masuala ya mafundisho yenye utata. Tunaongelea wanatheolojia maarufu kama vile Leonardo Boff (Brazil), Charles Curran (America), Hans Küng, Karl Rahner na wengineo ambao walikiri uwezo wa Ratzinger na kukaa pembeni.
Aidha, Pd. Dkt. Kireti katika homilia yake ametaja tunu na sifa kedekede za Benedicto XVI Papa, kuwa alikuwa anatambulika kwa unyenyekevu, upole, wema na pia kama mtu wa karama nyingi. Aliandika vitabu vingi sana vya theolojia; aliongea lugha kadhaa na alikuwa mcheza piano aliyesifika hasa katika kucheza simphonia za Mozart kwenye piano. Hizi karama zote alizitumia kuinjilisha na kuwafanya wengi wamjue na kumpenda Kristu, kama mtumishi mwaminifu anayewapa watu aliokabidhiwa mahitaji yao kwa wakati wake.
Tumesoma katika injili ya Luka: “Heri yake mtumishi huyo ikiwa Bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo; Hakika atamweka aitunze mali yake yote” (Lk 12:43-44). Benedict XVI Papa alijitahidi kuishi injili hii kwa mafundisho na matendo yake.
Baba Mtakatifu Fransisko akiaga mwili wa marehemu Benedicto XVI Papa
Tumwombee katika ibada hii ya Misa Takatifu, leo anapozikwa huko Roma -Vaticani, Mungu ampokee kwake na kumpa tuzo ya milele.
Baada ya maadhiisho ya Misa Takatifu, Baba Gambera wa Seminari Kuu ya Familia Takatifu Mwendakulima Msgr. Pius Rutechura naye alitoa neno juu ya Maisha ya Benedcto XVI Papa akisema: Tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya Benedicto XVI Papa katika Kanisa hasa nyakati zetu hizi. Kwa upande wa malezi na makuzi ya kipadre ametuachia urithi mkubwa. Uwezo wake kifikra, unyenyekevu na msimamo thabiti katika kutetea tunu za imani ni urithi mkubwa wa kutusindikiza katika safari ya wito wa kipadre. Tuendelee kumuenzi kwa kusoma na kuchambua maandishi yake ya kiteolojia.
Aidha, Msgr. Rutechura alisema, alibahatika kukutana na Papa Benedicto XVI Papa mara kadhaa na alijifunza mengi kutokana na usikivu wake na ufasaha wa kujibu maswali wakati wa adhimisho la Mwaka wa Padre. Katika Himizo lake la ‘Kitume Africae Munus’ baada ya Sinodi ya Pili Juu ya Africa, alisisitiza kuwa tunayo mengi ya kujifunza ili tuzidi kuimarisha utume wa upatanisho, haki na Amani katika Bara la Africa.
Alimalizia kwa kusema, kwa heri Baba Benedicto XVI Papa; kama ulivyotuasa, “Usafi wa moyo ndio unaotuwezesha kuona,”/ “Purity of heart is what enables us to see,” tunakuombea ufunguliwe milango ya Paradizo.
Raha ya milele umpe ee Bwana!Na mwanga wa milele umwangazie,Apumzike kwa amani,Amina.
Tafakari hii imeripotiwa kwenu nami Frt. Francis Tumaini wa Jimbo Katoliki Moshi ninayesoma Masoma ya Falsafa Katika Seminari Kuu ya Familia Takatifu – Mwendakulima (Kahama - Tanzania)