Baba Mtakatifu Fransisko amteua Padre Wilbroad Henry Kibozi, Makamu Gambera Seminari Kuu ya Kitaifa ya Familia Takatifu - Mwendakulima, kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Tanzania.
Mhashamu Askofu C. Ndizeye (kulia) na Mheshimiwa Monsinyo P. Rutechura (kushoto), walezi na waseminari wa Familia Takatifu - Mwendakulima; wakimpongeza Askofu Msaidizi Mteule wa Jimbo Katoliki Dodoma Padre W. H. Kibozi (katikati). (Picha: Frt. Emmanuel Nguvu)
Baba Mtakatifu Fransisko amemteua Padre Wilbroad Henry Kibozi kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma. Taarifa hiyo imetolewa rasmi kwenye vyombo vya habari na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tarehe 12 Februari 2024.
Kanisa Katoliki nchini Tanzania, kwa namna ya pekee Familia ya Mungu Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, wanatawaliwa na furaha kubwa kumpata Askofu Msaidizi katika Jimbo hilo. Kwa nafasi ya pekee, shangwe zatawala kwa Walezi na Waseminari wa SEMINARI KUU YA KITAIFA YA FAMILIA TAKATIFU - MWENDAKULIMA, iliyopo Jimbo Katoliki la Kahama, kwa Mheshimiwa sana Padre W. H. Kibozi kuwa mwanajumuiya wa seminari hiyo. Hadi uteuzi wake, Padre W.H. Kibozi alikuwa Makamu Gambera, Mwalimu na Mlezi wa Seminari hiyo kwa muda wa miaka 4, kuanzia 2020 mpaka 2024.
Mapadre wakimpongeza Askofu Msaidizi Mteule wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma. (Picha: Frt. Emmanuel Nguvu)
Mhashamu Askofu Christopher Ndizeye, Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama, alifikisha rasmi taarifa hiyo ya Uteuzi wa Padre W. H. Kibozi kuwa Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dodoma. Jumuiya ya Seminari ya Familia Takatifu ilipokea kwa furaha kubwa sana na shukrani kwa Mungu kwa Makuu aliyowatendea. Baba Askofu Christopher Ndizeye alitualika kumwombea Askofu-Msaidizi Mteule katika utume wake huo mpya.
Pia, Gambera wa Seminari, Mheshimiwa sana Monsinyo Pius Rutechura, alieleza furaha yake kubwa iliyotawaliwa na shukrani kwa Mungu na matashi yake mema kwa Askofu-Msaidizi Mteule wa Jimbo Kuu la Dodoma. “Historia imeandikwa katika seminari yetu japokuwa katika uchanga wetu tumepewa neema hiyo ya kupata tunda hilo kubwa katika Kanisa,” alisema Monsinyo Pius Rutechura. Hivyo, ameweka wazi kuwa KAMPENI YA KWARESMA 2024 ya seminarini hapo, ambayo pia huwezeshwa na baadhi ya marafiki wa Seminari, itakuwa kwa ajili ya kuwezesha Uaskofisho utakaofanyika katika Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, tarehe 12 Mei 2024.
WASIFU: Mheshimiwa sana Padre Wilbroad H. Kibozi, alipewa Daraja Takatifu ya Upadre mnamo tarehe 9 Julai 2010 katika Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma. Alikuwa Paroko Msaidizi wa Lumuma 2010-2012, Mkurugenzi wa Miito wa Jimbo Kuu la Dodoma 2012-2014, Muungamishi wa Nyumba ya Malezi Livorno, Italia 2017-2019, Mlezi wa Waseminari Chuo Kikuu cha Jordan (JUCO), Morogoro 2019-2020, na tangu hapo (2020) amekuwa Makamu Gambera wa Seminari Kuu ya Familia Takatifu - Mwendakulima mpaka kufikia uteuzi wake.
Waseminari wa Familia Takatifu - Mwendakulima, wakimpongeza Askofu Msaidizi Mteule wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma. (Picha: Frt. Emmanuel Nguvu)
Historia imeandikwa katika Jimbo Kuu la Dodoma; Historia imeandikwa katika Seminari Kuu ya Kitaifa ya Familia Takatifu – Mwendakulima. Mheshimiwa sana Padre W. H. Kibozi ndiye Askofu Msaidizi wa kwanza katika Jimbo Kuu la Dodoma; pia, kwa Seminari ya Familia Takatifu, anaiandikia historia ya kutoa Askofu Mteule kwa mara ya kwanza kabisa tangu kuanzishwa kwake rasmi tarehe 5 Disemba 2020.
Imeletwa kwenu na Frt. Augustine J. Soka na Frt. Francis J. Tumaini, waseminari wa Theolojia ya Kwanza, Seminari ya Familia Takatifu - Mwendakulima